Youth Partnership CountryWide (YPC)

Vijana, Wenzetu Wanakimbia Tuamke

Bila shaka upo salama, hongera kwa starehe za hapa na pale, kama una matatizo tumia busara na maarifa kuyatatua, omba utapewa, tafuta utapata, na usikate tamaa.

Namshukuru Mungu kwa ninachokipata kila inapoitwa leo ukiwemo uhai, nazidi kutafuta nisivyonavyo, maisha bora kwangu na kwako yanawezekana, shida zinavumilika lakini umasikini haukubaliki.

Pole kama unataabika popote ulipo kwa kutokuwa na kipato cha uhakika, jipe moyo kwamba ipo siku na wewe hutajiuliza utapata vipi fedha, ila utazitumia vipi, wapi na ikiwezekana na nani.

Kama huna ajira tambua kwamba, wewe ni miongoni mwa mamilioni ya Watanzania hasa vijana wanaohangaika kutafuta ajira kila inapoitwa leo na sidhani kama neno mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe ni msamiati kwako.

Kuna vijana wenye ujuzi wa fani mbalimbali lakini hadi sasa ugumu wa maisha umekuwa sehemu ya maisha yao, na wapo pia ‘waliopikwa’ kinadharia zaidi, wamehitimu shule za msingi, sekondari na hata vyuo lakini kwa kuwa waliandaliwa kuomba ajira, bado ni tegemezi, wametuma maombi hadi wamechoka, maisha mazuri kwao ni nadharia tu.

Wengi wakiwemo wanasiasa, viongozi wa Serikali, wasomi na watu wa kada tofauti wanazungumzia umasikini na ukubwa wa tatizo la ajira lakini hawataji kiini cha tatizo.

Mapema wiki hii wabunge wamezungumza mambo mengi kuhusu elimu ya nchi hii, ni wangapi wameeleza umuhimu wa somo la ujasirimali kwenye mitaala kuanzia elimu ya msingi?

Watanzania hawawezi kukombolewa kwa ongezeko la madarasa, maabara, nyumba za walimu au mishahara mizuri kwa walimu. Kuna kitu kinakosekana kwenye mitaala yetu, dunia imebadilika, tunapaswa kubadili mtazamo wa wahitimu shuleni na vyuoni, watoke huko wakiwa wameandaliwa kujiajiri si kuajiriwa.

Vijana wanaambiwa wachangamkie fursa za kujiongezea kipato , lakini hao wanaosema hivyo wanajifanya hawajui kuwa, mitaala ya shule za msingi na hata sekondari haiwaandai wahitimu kuwa wajasiriamali, au wawekezaji.

Leo mhitimu wa darasa la saba anaanzisha saluni, anafungua genge la mboga au duka, au analazimika kuwa mchuuzi wa bidhaa lakini shuleni hakufundishwa chochote kuhusu namna bora ya kufanya biashara, ubunifu wa biashara, namna ya kupata mtaji na masoko.

Wamachinga wangapi wanafahamu kanuni za kufanya biashara katika mazingira ya ushindani, umuhimu ubunifu, kuthubutu, kutafiti masoko ndani na nje ya nchi, kufanya biashara kwa mtandao, namna bora ya kujitangaza, namna ya kuongeza wigo wa mtaji nk?

Mfumo wa sasa uchumi ni wa kibepari, suala la biashara halikwepeki, mtaala wa elimu Tanzania umelizingatia hilo? Ni lini mtoto wa Tanzania ataanza kufundishwa biashara tangu akiwa shule ya msingi ili aweze kujiajiri akihitimu darasa la saba, sekondari au chuo?

Kutoingiza ujasiriamali kwenye mitaala ni kuukataa ukweli, kujidanganya, na kuishi kwa mazoea, Watanzania tubadilike, Wenzetu wanakimbia, tuamke. Siku njema.

Source: http://www.habarileo.co.tz/